Tabia Tano Za Kujijengea Ili Kuwa Na Maisha Mazuri.
Huwa tunafikiri maisha mazuri ni pale tunapopata kupata yale makubwa tunayotaka. Hivyo tunaweka juhudi zetu zote kuyapata, lakini tukishayapata ndiyo tunagundua kwamba tulichokuwa tunategemea siyo sahihi.
Kila kitu nje yako kinaweza kubadilika na kuwa kama utakavyo, lakini kama ndani yako utabaki kama ulivyokuwa, hutaweza kufurahia mabadiliko hayo ya nje.
Hivyo hatua ya kwanza na muhimu ya kuwa na maisha mazuri, ni kwa kujijengea tabia ambazo ni nzuri, tabia ambazo zinafanya maisha yako kuwa bora na tulivu kwenye kila hatua ya maisha hayo.
Miaka mingi iliyopita, Mwanafalsafa Seneca alioona changamoto hii kwa walio wengi, wakishindwa kujua ni jinsi gani wanaweza kujenga maisha mazuri kwao. Hivyo kwenye moja ya barua zake kwa rafiki yake Lucilius, aligusia hili la kuwa na maisha bora na kutaja tabia ambazo mtu anapaswa kujijengea.

Seneca alitushauri hili akiwa anajua kabisa, kwa kuwa yeye ni mmoja wa wale waliotoka chini kabisa na kufika ngazi za juu kifedha na hata kisiasa. Hivyo aliona ni jinsi gani mambo ya nje hayawezi kuleta maisha mazuri kwa mtu.
Do you ask me what this real good is, and whence it derives? I will tell you: it comes from a good conscience, from honourable purposes, from right actions, from contempt of the gifts of chance, from an even and calm way of living which treads but one path. – Seneca.
Ili kuwa na maisha mazuri, Seneca anashauri tujijengee tabia hizi;
Moja; dhamiri njema.
Haijalishi unafanya nini, wala haijalishi matokeo gani unayoyapata, bali kilicho muhimu ni dhamiri iliyo ndani yako. Nia ya wewe kufanya kile unachofanya ni muhimu kuliko unachofanya au matokeo unayoyapata.
Mara nyingi tunapofanya kitu, huwa tunaanza kuyaangalia maslahi yetu binafsi, tunakwenda kupata nini. Tunasukumwa zaidi na matokeo ya mwisho kwa sababu ndiyo tunachoangalia.
Hiki ndiyo chanzo cha wengi kukata tamaa, hasa pale matokeo ya mwisho yanapochelewa au yasipokuja kabisa.
Ili kuwa na maisha mazuri, anza na dhamiri njema. Chochote unachofanya, kwanza angalia ni mchango gani unatoa kwa wengine kabla hata hujaangalia wewe unapata nini.
Ndiyo ni lazima kuwe kuna kitu unapata, lakini huo haupaswi kuwa msukumo pekee kwako kufanya. Angalia wengine wananufaikaje na kile unachofanya. Kwa njia hii hata kama hutapata matokeo uliyotegemea, angalau utaona wale walionufaika na kile ulichofanya.
Pia itakuzuia kufanya yasiyo sahihi. Tumekuwa tunaona mara kwa mara watu waliofanikiwa kuja kugundulika walitumia njia zisizo sahihi na hilo linapelekea wapoteze mafanikio yao.
Wewe unapoanza na dhamiri njema, inakuzuia kufanya yale yasiyo sahihi, hivyo mafanikio yoyote unayoyapata, hakuna anayeweza kukunyang’anya kwa sababu ya njia ulizotumia.
Mbili; kusudi lenye heshima.
Kuna kitu ambacho huwa unapata msukumo mkubwa wa kukifanya ndani yako. Huwezi kuvumilia unapoona kitu hicho hakipo sawa na upo tayari kukifanya hata kama hakuna anayekulipa. Unapokuwa unafanya kitu hicho, unasahau kabisa muda, unaweza hata ukapitisha muda wa kula kwa sababu ulikuwa unafanya kitu hicho.
Hicho ni kitu ambacho kinatokana na kusudi ambalo liko ndani yako. Kusudi la mtu ni kama moto unaowaka kwenye nyasi, huwa hauzimi mpaka pale nyasi zinapoisha. Hata zikibaki kidogo, moto huo huendelea kuwana na kusambaa.
Watu wamekuwa wanakimbizana na kufanya yale ambayo kwa nje yanaonekana yanalipa, lakini ndani yao hawavutiwi kuyafanya. Wanafanya kwa sababu ya fedha na sifa. Kwa sababu inalipa vizuri na pia inampa hadhi kwenye jamii. Watu hawa wanaweza kupata kila kitu, lakini bado maisha yao yakawa na upungufu mkubwa.
Hakikisha unalijua kusudi lililo ndani yako na kulifanyia kazi. Hata kama siyo kazi yako kuu, usilizike kabisa kusudi hilo. Maana kadiri utakavyokutana na hali zisizo sahihi kwenye eneo ambalo ndiyo kusudi lako, utajisikia vibaya, utaona ungeweza kuwa na mchango wa tofauti kwenye eneo hilo.
Isikilize nafsi yako, inajua mengi kuhusu wewe, inajua kusudi lako, usilifiche, lifanyie kazi kama unataka kuwa na maisha mazuri.
Tatu; hatua sahihi.
Watu watakujua kupitia yale unayofanya, siyo unayosema utafanya, siyo hisia zilizokusukuma kufanya na wala siyo nia yako katika kufanya, bali kile hasa unachofanya ndiyo kinachogusa maisha ya wengine.
Hivyo basi, unapaswa kufanya kile kilicho sahihi mara zote, bila ya kujali kuna anayeona au la. Chochote kisichokuwa sahihi unachofanya, wewe utajua siyo sahihi na hilo litakusumbua.
Hata kama utapata kile unachotaka, kama hukufanya kisicho sahihi, hilo litaendelea kukuwinda na hivyo hutaweza kuwa na maisha mazuri.
Mara zote fanya kile kilicho sahihi, hata kama hakuna anayeona, kwa sababu huwezi kujidanganya mwenyewe. Kile unachofanya ni kura unayopiga kwenye aina ya mtu unayekua. Ukifanya kilicho sahihi mara zote, unakuwa mtu sahihi.
Nne; kuwa tayari kwa lolote.
Ukishajiambia huwezi kuishi bila ya kuwa na kitu fulani, tayari umeshayaharibu maisha yako. Asili huwa inafanya mambo yake kwa namna yake yenyewe, huwa haifuatishi matakwa yetu.
Hivyo inaweza kuchukua chochote ambacho unacho, iwe ni mtu unayempenda, iwe ni mali ulizotafuta usiku na mchana, iwe ni cheo ambacho umesota muda mrefu kukipata.
Asili haijali, ukifika wakati wa kuvuna inavuna kama itakavyo.
Hivyo kama unataka kuwa na maisha mazuri, kuwa tayari kupoteza chochote ulichonacho sasa, kwa wakati wowote, hata sasa. Hiyo inajumuisha maisha yako pia, asili inaweza kuyaondoa wakati wowote.
Yale unayoona yakitokea kwa wengine, jua kwa hakika yanaweza kutokea na kwako pia, tena kwenye wakati ambao hujajipanga. Hivyo badala ya kujidanganya muda wako bado na kisha ukakumbwa na mshangazo, jiandae kupoteza kila ulichonacho.
Hili litakusaidia kwa njia mbili;
Njia ya kwanza utakitumia kitu vizuri kwa wakati huu ambapo unacho, kwa kuwa unajua unaweza kukipoteza muda wowote. Fikiria umeambiwa leo ni siku ya mwisho, utapoteza muda kwa yasiyo muhimu? Kujua unaweza kupoteza kitu wakati wowote kinakifanya kitu hicho kiwe muhimu zaidi kwako.
Njia ya pili ni kutokuumia pale unapopoteza kitu hicho, kwa sababu ni uhakika utakipoteza, ila hujui lini. Kinachowaumiza watu wanapopoteza kitu ni kwa kuwa kinatokea wakati ambapo mtu hategemei. Chukua mfano wa misiba ya aina mbili, msiba wa kwanza ni wa mtu wako wa karibu sana, ambaye ameumwa na kulala kitandani kwa muda mrefu. Msiba wa pili ni wa mtu wa karibu ambaye asubuhi umeongea naye na mchana umepata taarifa kuwa amepata ajali na kufa. Taarifa ipi inakuumiza zaidi? Wote ni watu wa karibu sana kwako, lakini anayekufa kwa ajali atakuumiza kuliko aliyeumwa muda mrefu. Unapokuwa unajua kwamba kitu kitapotea, kinapopotea unajikumbusha kwamba ulijua hilo, na hapo maisha yanaendelea.
Tano; maisha tulivu.
Watu wengi wamekuwa hawana maisha bora wala hawapati wanachotaka kwa sababu hawana utulivu. Kila wakati wanahangaika na vitu visivyokuwa na umuhimu kwao. Kila wanaposikia kuna kitu kipya wanaacha walichokuwa wanafanya na kwenda kwenye kitu hicho kipya.
Inachukua muda, mtu anajikuta amehangaika na mambo mengi, lakini hakuna matokeo anayoweza kuonesha kwamba ameyapata.
Maisha tulivu utayapata kwa kuleta pamoja haya tuliyojifunza hapa, jua kusudi lililo ndani yako, kuwa na dhamiri njema ya kuwasaidia wengine kisha chagua kile utakachofanya kutimiza hayo mawili.
Ukishachagua utakachofanya, fanya hicho pekee na acha kusumbuka na mambo mengine. Kuna njia nyingi za kufika kule unakotaka kufika, lakini hutaweza kufika kama kila wakati unajaribu njia mpya. Unachohitaji ni kuchagua njia moja na kisha kuifuata hiyo.
Unapoacha kuhangaika na mambo mengi unapata utulivu mkubwa ndani yako, unapata muda wa kujua kile unachokifanya kwa kina na kuweza kukifanya kwa viwango vizuri. Hilo linapelekea wewe kuweza kutoa huduma bora kwa wengine huku pia ukipata unachotaka.
Usiache njia uliyochagua kwa sababu unaona inakuchelewesha wakati wengine wanawahi kwenye njia zao. Wajibu wako ni kuchukua hatua iliyo sahihi, matokeo yatakuja yenyewe, kwa wakati wake.
Nenda kaweke kwenye matendo haya uliyojifunza, kazana kujijengea tabia hizi tano kama bado hujawa nazo, na kama tayari unazo, endelea kuziimarisha kila siku. Kwa kuwa na tabia hizi, utaweza kuwa na maisha mazuri bila ya kujali nini kinachoendelea, kwa sababu ndani yako unakuwa na utulivu mkubwa huku ukichukua hatua sahihi na ukiwa tayari kwa lolote.
Karibu tuendelee kujifunza na kuishi misingi ya falsafa ya Ustoa kupitia mtandao wetu wa Falsafa Ya Ustoa Tanzania, tembelea www.ustoa.or.tz
Makala hii imeandikwa na Dr Makirita Amani, ambaye ni daktari wa binadamu, kocha wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali.
makirita@ustoa.or.tz / 0717396253