BARUA 11; Aheri Kudhihakiwa na Kutukanwa Wakati Ukitenda Mambo Yenye Tija
Endelea Kukazana Kutenda Yaliyo Mazuri kwa Jamii Yako
Nimekutana na watu wengi ambao wamekata tamaa pale walipoanza kuandika au kushirikisha maarifa mtandaoni na watu wakawajia juu na kuwasema “mnachokifanya ni upotevu wa muda, mnaandika au kufundisha vitu msivyoviishi” au mnasoma vitabu vingi lakini hambadiliki au hakuna anayesoma vitabu mnavyoandika. Kauli kama hizi zimewakatisha tamaa waandishi na walimu wengi ambao huenda maandishi au mafundisho yao ni tija kwa jamii sasa na kizazi kijacho ila wanakatishwa tamaa na watu wanaochukia mambo mazuri.
Chochote kilicho kizuri katika maisha huwa kinapingwa au kupatikana kwake ni gharama au mapambano makubwa. Utaona utajiri, kupata hekima, ufahamu ni hali ambazo haziji kirahisi bali kwa kujitoa, kujifunza, kuishi na kupambana. Ndivyo katika mambo yote mazuri ambayo watu hufanya basi wapo wengi ambao hawatapendezwa nayo. Ijapokuwa mabaya hupewa nafasi kubwa na kusifiwa zaidi. Hili linawakatisha wale wote watendao mazuri kuwa mbona tunatenda yaliyo tija ila hakuna anayejali au kushituka na kupongeza mazuri ?.
Jamii zetu toka kale zimefanywa kuvutwa zaidi na mambo yaliyo hasi au mabaya kuliko mambo yaliyo mazuri. Utaona namna habari mbaya kukuhusu wewe zitakavyoweza kusambaa kwa haraka kuliko habari zilizo njema kukuhusu wewe. Ona siku hizi namna picha za faragha za watu zinapovuja mtandaoni watu wanavyohimizana kuzisambaza na kuzitapanya zaidi. Ila si kweli kuwa hakuna mambo mazuri ambayo yangewezwa kutapanywa kama zilivyo habari mbaya. Sasa kwa wale watendao yaliyo mazuri hukatishwa tamaa kwa kuona juhudi na kujituma kwao kutenda mazuri bado watu wanawatusi na kutojali ingawa mazuri hayo kuwa na manufaa kwa jamii.
Chagua kutenda mazuri na yaliyo na tija hata kama hakuna anayejali au kupendezwa nayo. Hii hatua ni ngumu na watu hushawishika kuacha mazuri na kuwa watu wabaya kwa kuwa mabaya mengi yanapendwa na watu wengi. Usiache kutenda mambo mazuri kwa watu, kwa jamii, kwa taifa na Dunia kwa ujumla. Marcus Aurelius anazungumzia haya katika kitabu chake cha “The Meditations” kwa nukuu “It is noble to do good and be insulted for it.” Hii ikiwa na maana “Ni lulu kufanya mazuri na kutukanwa kwa ajili ya hayo.
Usikatishwe tamaa kwa kuwa unachokifanya hakuna anayekupongeza au kukushukuru licha yaliyo mabaya hupigiwa debe na kushangiliwa. Unahitaji kuendelea kutenda mazuri na yenye faida maana Dunia ina uhaba na watu wenye nia njema, wenye kusaidia wengine, walio tayari kuingia gharama ya kutengeneza njia kwa ajili ya wengine na walio tayari kuteketea ili wengine waishi vizuri hapo baadaye. Ni raha ilioje kuwa katika orodha ya watu ambao wamenia na kuendelea kutenda mazuri kwa jamii na wewe ukiwemo ?
Aheri utukanwe wakati jambo au unachokifanya hakifishi mtu, hakidhuru mtu au hakileti athari hasi kwa watu. Matendo mema unayoyatenda huacha alama njema mara baada ya ukomo wa maisha yetu. Mabaya hudumu muda mfupi ila mema huenda miaka mingi yakikumbukwa na vizazi vingi. Ingawa mema ukiwa hai watu hawawi tayari kusema ila mema huendelea kudumu hata baada ya kifo cha mtu. Usiache kutenda kitu kilicho na tija kwa kukatishwa na watu ambao wanataka uache hilo. Nipo tayari kutukanwa au kudhihakiwa katika kitu chochote nachokifanya kilicho na manufaa.
Dkt. Raymond N Mgeni
+255 676 559 211